Friday, December 18, 2015

Serikali kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kutumia vyeti vya kughushi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) ameiagiza Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kutumia vyeti visivyo vyao kupata ajira Serikalini.
Mhe. Kairuki aliyasema hayo jana alipotembelea Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu–UTUMISHI ikiwa ni muendelezo wa ratiba yake ya kutembelea Idara/Vitengo vya Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
“Watumishi wote waliobainika kupitia Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) kutumia vyeti visivyo halali kwao wachukuliwe hatua stahiki” Mhe. Kairuki amesema.
 Aidha, Mhe. Kairuki amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI Bw. Emmanuel Mlay kutafuta Ufumbuzi wa kumalizana na tatizo la watumishi wanaotumia vyeti vya kughushi.
“Muwasilishe vyeti vyao Baraza la Mitihani kwa ajili ya uhakiki na baada ya uhakiki muwachukulie hatua stahiki watumishi wanaoonekana kutumia vyeti visivyo halali kwao” Mhe. Waziri alisisitiza.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI Bw. Leonard Mchau alisema kuwa Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma imehakiki jumla ya watumishi 704 ambao kati ya hao watumishi 219 baada ya vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani wamegundulika kuwa waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi.
Bw. Mchau aliongeza kuwa baadhi ya watumishi hao walioonekana kughushi vyeti ili kujipatia ajira Serikalini wamekimbia vituo vyao vya kazi.
Bw. Mchau aliwaasa wananchi kuepuka mchezo wa kughushi vyeti ili kujipatia ajira Serikalini.
“Ni kosa la jinai kughushi vyeti kwa lengo la kujipatia kazi hivyo endapo utagundulika umeghushi vyeti utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.”  Bw. Mchau alifafanua.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma inaendelea na zoezi la uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wote wa Umma nchini na matarajio ni kuwahakiki watumishi wote.Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) (kushoto), akipewa ufafanuzi kuhusu madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Umma (arrears) kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI Bw. Leonard Mchau. Katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI Bw. Emmanuel Mlay.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) (kushoto), akitoa maelekezo kwa Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu-UTUMISHI. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (Mb) (kushoto), akipewa ufafanuzi kuhusu fomu za madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Umma (arrears) .

No comments:

Post a Comment